March 27, 2018

Ufanye Nini Kama Umesahau Kumeza Vidonge Vya Majira?


Related image 
Vidonge vya uzazi wa mpango ni miongoni mwa njia za uzazi wa mpango ambazo zinatumiwa na wanawake kuzuia mimba. Vidonge hivi vya kumeza vipo vya aina mbili, ya kwanza huwa imebeba viambata viwili vya vichochezi (hormones) aina ya estrogen na progestin.


Aina ya pili ni vidonge vya Progestin pekee (POP) au “mini pill” na huwa ina kiambata cha progestogen pekee. Vidonge hivi viko 28 katika pakiti moja na hutumiwa kimoja kila siku.

Aina zote hufanya kazi ya kuzuia upevushwaji wa kijiyai cha kike katika ovari, huzuia mbegu ya kiume kukifikia kijiyai kwa kufanya maji maji ya ukeni kuwa mazito na kuzuia kijiyai kilichoungana na mbegu ya kiume kujipachika katika nyumba ya uzazi.

Ni kawaida wakati mwingine kuifanya hedhi kupungua na kupunguza maumivu wakati wa hedhi. Inapotokea mtumiaji wa vidonge hivyo amesahau kumeza hujikuta akipata hofu kwa kuhofia pengine itashindwa kufanya kazi ya kuzuia mimba.
 Image result for vidonge vya majira
Hali ya kusahau kumeza hujitokeza hasa kwa wanawake wanaofanya kazi nyingi zinazochosha akili ikiwamo wafanyakazi wa viwandani, walimu, wanafunzi, wanamuziki na watafiti.

Pale inapotokea umesahau kumeza vidonge vya majira, utakapokumbuka tu haraka chukua kidonge hicho na umeze papo hapo.
Ikitokea hukukumbuka kumeza mpaka kufikia siku inayofuata usihofu, endelea kutumia na meza vidonge viwili vya siku hiyo uliyokumbuka na viwili tena siku inayofuata.

Baada ya hapo utaendelea na utaratibu wa umezaji kama kawaida, ambao huwa ni kidonge kimoja kila siku.

Kama utasahau kumeza zaidi ya vidonge viwili ni vizuri kufika katika huduma za afya idara ya baba, mama na mtoto katika kitengo cha uzazi wa mpango au fanya mawasiliano na daktari wako.

Ni kawaida kwa mtoa huduma za afya kukushauri umeze kidonge kimoja kila siku mpaka inapofika siku ya jumapili. Katika hatua hii utahitajika kufungua na kutumia pakiti mpya ya vidonge vya majira.
 Related image
Au unaweza kuelezwa kurudisha au kuvitupa pakiti ya vidonge ulivyokuwa ukitumia na kusahau kumeza, utapewa nyingine mpya utakayotumia kwa kufuata utaratibu wa umezaji kama inavyohitajika.

Muda wowote unaposahau kutumia vidonge hivyo ni lazima utumie njia nyingine ya uzazi wa mpango mpaka utakapo maliza pakiti ya vidonge vya majira.
Kumbuka unaposahau kumeza kidonge unaongeza nafasi ya kuchoroposhwa kwa kijiyai cha kike katika kokwa za kike (ovary), hivyo kukuweka katika hatari ya kupata mimba.

Ingawa kama utasahau kumeza kidonge cha siku kati ya vidonge saba vya kundi la mwisho katika ya vile 28 vinavyotumika kimoja kila siku, haita kuhatarisha kupata ujauzito.

Hii ni kwasababu vidonge hivyo saba vya mwishoni huwa na kiambata mfu tu ambacho hakina uwezo wa kuzuia uchoroposhwaji wa kijiyai cha kike. Inapotokea umesahau kumeza na hukuona siku zako, ni vizuri kufanya kipimo rahisi cha kutambua kama mimba imetungwa.

Image result for vidonge vya majira
Kama hukuona siku zako kwa muda wa siku mbili na huku umemeza vidonge vyako vyote kama mpangilio wake unavyotaka, itakulazimu kupima kipimo cha kuchunguza kama umepata mimba.

Ni vizuri kuweka utaratibu wa kumeza vidonge vya majira muda ambao haujatingwa na kazi nyingi ukiwamo nyakati za jioni au asubuhi, weka alamu ya simu au saa itakayokushtua.Share: