Madaktari huunganisha habari unayotoa
kutoka kwenye dalili unazohisi, historia ya maradhi yaliyowahi kukusumbua,
uchunguzi wa mwili wako pamoja na kufanyiwa vipimo ili kugundua maradhi au
hatari ya kupata maradhi fulani kama kisukari.
Kupima afya ni muhimu kwa wanaume, hata
kama hawana dalili za magonjwa. Madaktari bingwa wa magonjwa ya tiba
wanapendekeza wanaume wafanyiwe uchunguzi wa afya kila mwaka.
Hata hivyo, kama mtu ana viashiria
hatarishi vya kupata magonjwa sugu kama kisukari, mtaalamu wa afya atamshauri
ni mara ngapi apime afya yake.
Kuna mambo ambayo ni muhimu katika umri
wowote na mengine ni muhimu zaidi katika umri mkubwa.
Madaktari huunganisha habari unayotoa
kutoka kwenye dalili unazohisi, historia ya maradhi yaliyowahi kukusumbua,
uchunguzi wa mwili wako pamoja na kufanyiwa vipimo ili kugundua maradhi au
hatari ya kupata maradhi fulani kama kisukari.
Ni vyema kumuuliza daktari wako kuhusu
vipimo unavyotakiwa kufanyiwa, kwa maana vipimo hutegemeana na umri, historia
ya matatizo ya afya katika familia, mtindo wa maisha unayoishi, vyakula
unavyokula, aina ya kazi yako na hali ya unywaji pombe na uvutaji tumbaku.
Unaweza kufanyiwa baadhi ya vipimo kama
shinikizo la damu kwenye chumba cha daktari. Vipimo vingine kama Kolonoskopi
(Colonoscopy) ambacho ni kipimo kinachotumika kupima saratani ya utumbo mpana,
huhitaji vifaa maalumu hivyo inawezekana vikafanyika chumba tofauti.
Vipimo vikubwa zaidi vya afya ya mwili
mara nyingi vinahitaji mgonjwa kukaa hospitalini hadi usiku mnene. Vipimo
vitafanyika kwenye mwili wako wote ili kuhakikisha huna tatizo lolote. Kama
unajisikia vizuri na majibu ya vipimo yameonyesha huna tatizo, basi utakuwa na
afya njema.
Kabla ya kufanyiwa vipimo daktari
anaweza kushauri usile vyakula vizito kama ugali kwa karibu saa 24, ili
kuruhusu baadhi ya vipimo kufanyika. Vipimo vitahusisha X ray za baadhi ya
maeneo ya mwili wako kama kifua, vipimo vya mkojo, vipimo vya kinyesi, vipimo
vya damu na vinginevyo.
Wakati unafanyiwa vipimo daktari anaweza
akawa anakuuliza maswali kadhaa. Na kama una kitu unachohisi ambacho si cha
kawaida unaweza kumwambia daktari wako akakufanyia uchunguzi; pengine anaweza
kukuandikia dawa nzuri kwa ajili ya maradhi yako. Vipimo gani muhimu kwa
wanaume?
SHINIKIZO
LA DAMU
Shinikizo la damu linapaswa kupimwa kila
unapofika hospitali kwa ajili ya matibabu.
Ikiwa una matatizo ya moyo na figo, na
kama una kiharusi, daktari wako atapendekeza uwe na shinikizo la damu la chini
zaidi kuliko watu wasio na matatizo.

Inawezekana ukaambiwa kuwa shinikizo
lako la damu hupanda kwa vile unazeeka. Hii ni kwa sababu mishipa ya damu
inazidi kuwa migumu kwa kadri umri unavyoongezeka.
Shinikizo kubwa la damu siyo zuri kwa
afya yako kwa kuwa linaongeza hatari ya kupata kiharusi, mshtuko wa moyo, moyo
kushindwa kufanya kazi, ugonjwa wa figo na kifo cha ghafla.
KUPIMA
LEHEMU
Kutokana na mfumo wa sasa wa maisha na
vyakula tunavyokula, uchunguzi wetu wa kiafya inabidi uhusishe kupima kiwango
cha kolesteroli (lehemu).
Kuwa na kiwango kikubwa cha kolesteroli
kuna maana ya kuwa na mafuta mengi kwenye damu, kitu kinachoweza kusababisha
kupata magonjwa ya moyo.
UZITO
NA KIMO
Mtu anapaswa kuwa na uzito unaofaa ambao
uko sawa na kimo kwa taratibu za kiafya. Njia sahihi ya kujua kama uzito na
kimo chako vipo vizuri kiafya ni kwa kutumia uwiano wa uzito na kimo (BMI).

Unaweza kutumia kikokotozi cha BMI na
kupata majibu. Kwa kawaida BMI chini ya 18.5 inaashiria upungufu wa uzito. BMI
kati ya 18.5 na 25 huashiria afya njema. Mtu mwenye BMI ya 30 au zaidi atakuwa
na uzito kupita kiasi.
UCHUNGUZI
WA TEZI DUME
Wanaume wenye miaka kuanzia 45 na
kuendelea, wanapaswa kufanyiwa vipimo vya tezi dume. Kipimo rahisi cha kwanza
kisicho na gharama ni daktari kuingiza kidole cha shahada katika njia ya haja
kubwa na kutomasa tezi dume. Akihisi tezi ni kubwa na ina vinundu, hii ni
ishara kuwa una saratani ya tezi dume.

Kipimo kiitwacho kitaalamu Prostate
Specific Antigen (PSA) ni kipimo cha damu kinachosaidia kugundua saratani ya
tezi dume.
UCHUNGUZI
WA UTUMBO MPANA NA PURU
Saratani ya utumbo mpana na puru (njia
ya haja kubwa) mara nyingi hutokea wakati kuna uvimbe usio wa kawaida kwenye
maeneo hayo.
Vipimo vya kolonoskopi vinaweza kugundua
uvimbe mdogo mapema na kuruhusu daktari kuweza kuuondoa kwa upasuaji kabla
haujakua.
Kinyesi kilichochanganyikana na damu
inaweza kuwa dalili ya mwanzo ya saratani ya utumbo mpana, hivyo kinyesi
kinaweza kupimwa kugundua kama kuna saratani hiyo.

Kama umri wako ni chini ya miaka 40,
daktari wako anaweza kukufanyia kipimo cha korodani. Daktari atakuambia ugeuze
kichwa na ukohoe, huku yeye akishika korodani zako kuangalia henia.
UCHUNGUZI
WA MACHO
Ni muhimu kwa wanaume kufanya vipimo vya
macho ili kuchunguza matatizo fulani ya macho. Vipimo vinaweza kupima uonaji na
afya ya macho yako. Kufanyiwa vipimo vya macho kunaweza kugundua matatizo ya
macho kama glaukoma, mtoto wa jicho.

UCHUNGUZI
WA MENO
Uchunguzi wa meno unahusisha kukagua
meno, fizi, kinywa, ulimi na limfu za shingo. Inashauriwa kufanya uchunguzi wa
meno kila baada ya miezi 6 ili kuwa na kinywa chenye afya bora. Ili kukamilisha
uchunguzi wa meno, inapaswa kuhusisha vipimo vya X ray. 

Na
Dr. Joachim Mabula