Thursday, May 30, 2013

TAHADHARI YA TISHIO LA MLIPUKO WA UGONJWA WA KUPOOZA (POLIO) TAHADHARI LA TISHIO LA MLIPUKO WA UGONJWA WA KUPOOZA (POLIO)


Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
imepokea taarifa mnamo tarehe
22 Mei 2013 kutoka Shirika la Afya
Ulimwenguni, (WHO) ya kuwepo
kwa mlipuko wa ugonjwa wa
kupooza (Polio) katika Wilaya ya
Fafi nchini Kenya.
Mpaka sasa kuna
mgonjwa mmoja bila kifo.

Ugonjwa wa Polio ni ugonjwa wa
kuambukiza unaosababishwa na
virusi vijulikanavyo kama “Polio
Virus”. Ugonjwa huu unaathiri
misuli na mfumo wa fahamu hivyo
kusabisha kupooza kwa viungo
hasa miguu na hata kifo. Ulemavu
huu ukishajitokeza huwa ni wa
kudumu. Waathirika wakuu wa
ugonjwa huu ni watoto hasa walio
na umri chini ya miaka mitano.

Hata hivyo ugonjwa huu
unazuilika kwa chanjo ya Polio
ambayo ni salama na inatolewa
bure na Serikali katika vituo vyote
vya huduma ya afya. Mtoto
aliyepata chanjo ya Polio anakuwa
amekingwa na ugonjwa wa Polio
kwa maisha yake yote.

Kutokana na taarifa hiyo ya kutoka
nchini jirani ya Kenya, baadhi ya
mikoa ina uwezekano mkubwa wa
kupata maambukizo ya ugonjwa
huo kufuatia ushauri wa kitaalam.
Aidha, mikoa hii mingine
inapakana na nchi jirani ya Kenya
na mingine ina mapungufu
yaliyopo katika hali ya chanjo ya
Polio. Mikoa hii ni pamoja na Dar
es Salaam, Pwani, Tanga, Arusha,
Manyara, Kilimanjaro, Mara na
Mwanza.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii,
imechukua hatua zifuatazo katika
kukabiliana na tishio la ugonjwa
huu:
· Kutoa taarifa ya
tahadhari ya ugonjwa huu
kupitia kwa Waganga Wakuu
wote wa Mikoa na Wilaya.

· Kuimarisha ufuatiliaji
wa ugonjwa huu kupitia kwa
Wataalamu wa Afya katika
Mikoa, Wilaya na maeneo ya
mipaka

· Kufuatilia kwa karibu
hali ya chanjo mikoani na
wilayani hususan ya Polio
hususani iliyo katika hatari
ya maambukizi.

· Kuhamasisha watoto
ambao hawajakamlisha
ratiba yao ya chanjo hususani
ya Polio au ambao
hawajapata ya chanjo hii
waweze kwenda vituo vya
karibu vya afya vya kutolea
chanjo.

Wizara inapenda kuchukua fursa
hii kutoa wito kwa Viongozi na
Watendaji wa ngazi zote kutoa
ushirikiano ili kuhakikisha kila
mtoto mlengwa anapata chanjo ya
Polio. Aidha Wizara inatoa rai kwa
wadau wetu, taasisi za dini, taasisi
zinazofanya kazi katika jamii na
vyombo mbalimbali kuhamasisha
watu wapeleke watoto wao
kwenye vituo vya huduma
wakapewe chanjo hii muhimu.

Chanjo hii ni salama na inatolewa
bila malipo.
Wananchi wanashauriwa kutoa
taarifa kwenye kituo cha huduma
za afya kilicho karibu mara
wanapoona au kupata taarifa ya
mtoto yoyote anayepata ulemavu
wa ghafla pasipo sababu yoyote.
Mtoto huyo apelekwe katika kituo
cha huduma za afya kwa
uchunguzi na hatua za haraka.
Imetolewa na;

Nsachris Mwamwaaja
Kitengo cha Mawasiliano
Serikalini
30/05/2013


0 comments:

Post a Comment